Jeshi la Polisi limewaua watu wawili wanaodaiwa kuwa ni miongoni mwa wanaofanya mauaji katika Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji, mkoani Pwani kufuatia oparesheni kali inayoendelea katika mkoa huo.
Akielezea tukio hilo Alhamisi hii, Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas amesema tukio hilo lilitokea Jumatano usiku katika msitu wa Ngomboroni Kata ya Ikwiriri, Wilaya ya Ikwiriri.
Kamishna Sabas alieleza Askari wakiwa na mtuhumiwa mmoja anayeshiriki katika mauaji hayo ambaye alikuwa amekamatwa baada ya mahojiano alikubali kwenda kuwaonyesha polisi mahali ambapo ni maficho ya wenzake.
“Baada ya kufika eneo la msitu wa Ngomboroni kikundi cha watu wanaokadiriwa kufikia watano walikurupuka kutoka kwenye kichaka na kuanza kukimbia ndipo polisi kwa tahadhari kubwa walianzisha mashambulizi na kufanikiwa kumjeruhi mhalifu mmoja kwa risasi, katika mashambulizi hayo mtuhumiwa aliyekuwa mkononi mwa polisi naye alijaribu kutoroka na hivyo kupelekea kumjeruhi kwa risasi hivyo idadi yao kufikia wawili,” alisema Sabas.
Aidha Kamishna Sabas amesema katika tukio hilo wamefanikiwa kupokonya silaha mbili aina ya SMG “Katika tukio hilo tumefanikiwa kupata silahab mbili aina ya SMG na shot gun moja pamoja na risasi 9 za SMG zilikuwa kwenye Magazine.”