Harmorapa: Kiboko ya mabishoo anayemtamani Wema Sepetu

harmorapa

SANAA ya muziki ni ajira inayolipa hasa ukiwa mjanja na kutambua kile unachokifanya.

Miongoni mwa wasanii chipukizi ambao ni wajanja na wanaokuja kwa kasi sasa ni Harmorapa. Watu pengine waliwahi kusikia hilo jina lakini walikuwa wakijiuliza Harmorapa ni nani? Jina lake kamili ni Athuman Omar mzaliwa wa kijiji cha Napata Magumuchila, Masasi mkoani Mtwara.

Ameanza kupata umaarufu mwishoni mwa mwaka jana kwenye mitandao ya kijamii baada ya kujitokeza na kudai kuwa anafanana na nyota wa muziki wa kizazi kipya ambaye yupo chini ya lebo ya Wasafi (WCB) ,Rajab Abdul ‘Harmonize.’ Utofauti wao upo katika aina ya muziki wanaoimba.

Harmonize anaimba mtindo wa taratibu na Harmorapa ‘anachana’ kwa lugha ya mtaani. Wengine wanasema ‘Rap’ au kufokafoka. Kitendo cha kujitokeza hadharani na kujifananisha na Harmonize kilizua gumzo kwenye mitandao. Wengine wakisema hafanani na wengine wakikubali hufanana na baadhi wakimtukana.

Kabla ya kujiita Harmorapa jina lake la awali la kisanii alikuwa akipenda kuitwa Jembe la Kusini. Lakini kitendo cha kufananishwa na Harmonize akaona atafute jina litakalofanana na msanii huyo wa WCB ambaye naye pia ni mzaliwa wa Kusini ingawa hawana undugu hata kidogo.

“Watu wengi wamekuwa wakinifananisha na Harmonize lakini ukweli sina hata undugu wala simfahamu,”anasema. Hata hivyo kufananishwa kwake na Harmonize kulizua ugomvi ambao mpaka sasa bado upo, na ulichochewa zaidi na dansa wa Nasib Abdul ‘Diamond’, Mose Iyobo aliyemfananisha Harmorapa na Nyani.

Ilikuwa hivi, mtangazaji wa kituo cha Redio cha Clouds ,Hamis Mandi ‘B Dozen’ aliweka ‘posti’ kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter juu ya mtafiti wa sokwe duniani, Jane Goodall. Iyobo akajibu kupitia mtandao huo kuwa “ Duh, noma sana ila mwambie kuna nyani anaitwa Harmorapa, angekuja kumfanyia utafiti na kujua tabia zake angetisha sana”.

Maneno hayo anasema yalimuumiza kupita kiasi. “Ni kitu ambacho kila nilipokuwa nikifiriki kiliniumiza moyo sana, kwa kweli siwezi kusahau na sijui kwa nini aliamua kuniita mimi Nyani, ilinifanya hata nitunge mashairi juu ya hilo neno”.

Anasema alimpa muda Iyobo kuomba radhi lakini hakufanya hivyo, na sasa ameamua kumuachia Mungu. Ila anasema kama atajitokeza kuomba radhi atamsamehe.

Kutokana na kuumia huko, aliamua kutunga wimbo unaofahamika kama ‘Kiboko ya mabishoo’ aliomshikirisha nyota mkongwe wa muzikiwa bongo fleva Juma Kassim ‘Nature’. Wimbo huo ameonesha hisia zake juu ya kile alichoitwa Nyani na yeye kumwambia kama yeye Nyani basi yeye (Iyobo) atakuwa ni Sokwe.

Huo ni wimbo wa pili tangu ameingia kwenye muziki huo. Wimbo wake wa kwanza aliutoa mwaka jana unaitwa Usigawe pasi lakini haukufanya vizuri. Tangu ajihusishe na muziki hajawahi kufanya shoo/ kutumbuiza kokote na kwa mara ya kwanza atafanya hivyo katika sikukuu ya Pasaka kwenye ukumbi wa ‘Dar Live Mbagala’.

“Nawaomba mashabiki wa muziki wanipokee kwa mikono miwili, nitakuwepo Dar Live Mbagala sikukuu ya Pasaka, nategemea muziki kuwa sehemu kubwa kuendesha maisha yangu,” anasema. Msanii huyo amekuwa mjanja akihangaika kuuza jina lake. Amekuwa akitafuta visa vitakavyomfanya kujulikana ili kutimiza lengo lake.

Pia, amekuwa akihusishwa kwenye mahusiano na wanawake maarufu nchini. Anasema, “Sio kwamba napenda kiki isipokuwa kila mnachokiona kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya mahusiano yangu kina ukweli ndani yake”.

Nyota huyo alizidi kujipatia umaarufu zaidi hasa kwenye tukio la aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye siku aliyozungumza na vyombo vya habari kuviaga ambapo alitishiwa bastola hali iliyomfanya msanii huyo kutimua mbio.

Wakati Nape ameshuka kwenye gari alijaribu kumsogelea ili amsalimie na mara alipoona mtu anayedaiwa ni usalama wa taifa akimnyooshea waziri huyo bastola alitoka ‘nduki’ hadi kwenye gari yake kwa hofu. “Unajua siku ile nilikwenda kumsalimia Waziri, sikutegemea kukutana na vitu kama vile lakini ndio maana nilikimbilia kwenye gari nione kinachoendelea,” anasema.

Ni wazi kuwa mbio hizo zilimfanya hata wasiomjua kufuatilia mtu huyo ni nani baada ya kuonekana kwenye video na picha mnato katika mitandao ya kijamii akikimbia kukwepa bastola hiyo. Pia, ilisababisha kuchorwa vibonzo vya kuchekesha juu yake akionekana anakimbia.

Kutokana na mbio hizo, ilimsaidia hivi karibuni kutangazwa kuwa balozi wa kinywaji cha Swala. Ingawa hakupenda kuzungumzia sana mkataba dhidi ya ubalozi huo akisema uongozi wake unajua zaidi. Ni msanii anayetabiriwa makubwa huko mbele kama ataendelea na juhudi zake za kuupaisha muziki wake.

Je, amewahi kukutana na Harmonize? “Niliwahi kukutana naye mara moja na kusalimiana kisha kila mtu akaendelea na mishe zake”. Usichokijua Harmorapa (24) ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watatu kwa upande wa mama yake lakini pia ni mtoto wa pili kwa baba yake.

Baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari Lukuledi mwaka 2010 alikuja Dar es Salaam. Mwaka 2013 akajiingiza kwenye biashara ndogo za uuzaji wa pochi za kina mama katika maeneo ya Mwenge. Hapo ndipo alipokutana na Meneja wake Irene Sabuka mwaka 2016 ambaye alikuwa mteja wake mkubwa wa pochi na ndipo kuamua kumweleza ukweli kwamba anapenda kuimba muziki.

“Akaniambia hebu imba nikusikie, nikaanza kuimba na ndipo akaamua kufanya kazi na mimi, na kutoa wimbo wa kwanza mwishoni mwa mwaka jana,”anasema.

Anasema muziki hakuanza siku za karibuni, alikuwa akipenda tangu akiwa anasoma Sekondari Masasi. Wakati huo alikuwa akivutiwa na wasanii wakongwe ambao pia wanaimba mtindo wake kama Farid Kubanda ‘Fid Q’, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Mikumi, marehemu Albert Mangwea, Juma Nature na wengine wengi.

Anasema alikuwa anatamani kuwa kama wasanii hao. Malengo Kama ilivyo kwa kila mtu mwenye ndoto zake, Harmorapa anatamani kwanza kuufanya muziki wake ujulikane ndani ya nchi nzima na baadaye aweze kuvuma kimataifa. Pia, anatamani kufanya kolabo na wasanii wakubwa na miongoni mwao ni Ali Kiba kwa upande wa Tanzania.

Na tayari amefanya naye mazungumzo hivyo anasubiri muda sio mrefu kuachia ngoma nyingine kali. Baada ya Ali Kiba anaota kufanya kazi na msanii wa Nigeria Tecno na Afrika Mashariki anampenda Prezo wa Kenya. Mapenzi Harmorapa anasema ameshawahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na wanawake wengi maarufu na kwasasa mpenzi wake ni msanii Amber Lulu.

Pia, anasema licha ya kuwa kwenye uhusiano na Amber hisia zake anatamani kukutana na Miss Tanzania mwaka 2006 Wema Sepetu kwani ni mwanamke anayemvutia. Changamoto Moja ya changamoto aliyowahi kukutana nayo na kumkatisha tamaa ni kitendo cha kutothaminiwa na watayarishaji wa muziki.

Anasema aliwahi kurekodi wimbo na kukabidhiwa mwaka uliofuata. Anasema kitendo hicho kinakera na kumpotezea mtu muda wake kwani unaporekodi unahitaji kukabidhiwa mapema wimbo wako ili upate muda wa kupeleka kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kuchezwa.

Jambo lingine anasema tangu ameanza kuwa maarufu anapata usumbufu mkubwa wa watu wakimpigia simu. Anasema kuna marafiki zake wamekuwa wakimuona kama anaringa, jambo ambalo sio kweli kwani yeye ni mtu wa watu isipokuwa amekuwa akipambana ili aweze kujenga jina.

Harmorapa anaomba kuungwa mkono ili kutimiza ndoto zake za muziki hasa ikizingatia kwamba ndio kwanza ameanza. Anategemea kazi hiyo kutimiza malengo yake ya maisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

mersin escort yeni