Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 01 Aprili, 2017 aliwaapisha wajumbe wa kamati maalum ya kuchunguza kiwango na aina ya madini yaliyomo kwenye mchanga wenye madini ulio ndani ya makontena yaliyopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.Hafla ya kiapo kwa wajumbe wa kamati hiyo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Harold Nsekela na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Kamati hiyo ya wanasayansi 8 walioteuliwa na Mhe. Rais Magufuli tarehe 29 Machi, 2017 inaongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Abdulkarim Hamis Mruma na itafanya kazi ya uchunguzi kwa siku 20 kisha kuwasilisha ripoti yake kwa Mhe. Rais.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amesema ameamua kuunda kamati hiyo yenye wasomi waliobobea katika masuala ya jiolojia, kemikali na uchambuzi wa kisayansi ili wawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50 ambao wanataka kujua ukweli kuhusu rasilimali yao ya madini.“Hivi sasa duniani kuna vita nyingi na vita mojawapo ni vita ya uchumi, kwa hiyo tunawatuma nyinyi mwende mkapigane vita hii katika sekta hii ya madini, mkawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50, mkapate ukweli wote na wala msikubali kuyumbishwa na mtu yeyote, tumieni utaalamu wenu, busara zenu, uzalendo wenu kwa Taifa na upendo wenu kwa Watanzania hasa masikini wenye shida nyingi”amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Dkt. Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kufanikisha kazi hiyo na ametaka wawe huru kutumia vitendea kazi vyovyote vinavyohitajika zikiwemo maabara mbalimbali za taasisi za Serikali na nyinginezo.
“Nendeni popote mnapohitaji kufanya kazi tutawapa ushirikiano, fungueni makontena popote yalipo, chukueni sampuli na mkazipime mjue kilichomo na naviagiza vyombo vya dola vihakikishe hakuna mtu atakayewakwamisha” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amesema baada ya kuunda kamati hii ya wanasayansi ataunda kamati nyingine ya wachumi na wanasheria kwa ajili ya kufanya tathmini na kuiangalia sera na sheria ya madini kwa lengo la kupata taarifa zaidi juu ya biashara ya madini hapa nchini.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Kihindu ya BAPS Swaminarayan Sanstha Duniani Mtukufu Mahant Swami Maharaj ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku 7.
Pamoja na kumshukuru kwa ujio wake hapa nchini, Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Jumuiya hiyo na amewaalika wafanyabiashara walio chini ya Jumuiya hiyo kuja nchini Tanzania kuwekeza katika viwanda, kilimo na shughuli nyingine za biashara na uwekezaji.
“Nimefurahishwa sana na ujio wako Mtukufu Mahant Swami Maharaj, sisi Tanzania tumekuwa tukishirikiana na Jumuiya ya Hindu tangu miaka mingi, nitafurahi kama mtaungana na juhudi za Serikali ya Tanzania kujenga viwanda, njooni mjenge viwanda na Serikali itawapa ushirikiano wowote mtakaohitaji” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mtukufu Mahant Swami Maharaj ambaye amefanya dua ya kuliombea Taifa na Rais, amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukutana nae na amemhakikishia kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya Jumuiya hiyo na Tanzania ulioanzishwa tangu enzi za utawala wa Awamu ya Kwanza ya Tanzania unaendelezwa na kukuzwa zaidi.