-
Je, yule kijana wa Tandale, Temeke, Mbagala mwenye fulana kubwa iliyoandikwa WCB ataweza kuingia kwa gharama hiyo? Jibu rahisi ni kwamba hatoweza.
Ni lazima afikirie ajue kwamba gharama anazotoza sehemu nyingine ziwe tofauti na Tanzania, au azifanyie gharama hizo kampuni kubwa za mitandao ya simu na vinywaji lakini si mtu binafsi.
Mara nyingi amekuwa akisema huko nje analipwa zaidi ya milioni mia moja, je, ni halali hata kwa Watanzania wenzake waliomfanya kuwa hapo alipo kuwatoza kiasi hicho cha fedha huku huyo anayemchukua akitarajia shoo yake iingiwe na watu wa hali ya chini wenye kiu ya kumuona?
Labda Naseeb Abdul mwenyewe ndiye aliyelazimisha ada hii, kama si yeye bali ni mameneja wake (Salam na Tale) basi wanamshauri vibaya na matokeo yake kutofanya shoo nyumbani kwake (Tanzania) kutamfanya apoteze kupendwa na mashabiki sababu ya umbali alioutengeneza.
Ikumbukwe kwamba watu hununua bidhaa ya mtu wanayempenda, mtu akichukiwa na bidhaa zake hususiwa.
Diamond na WCB ni biashara ya Naseeb Abdul, hivyo basi Naseeb Abdul hatakiwi kuthamini sana fedha na kusahau mashabiki zake waliomfanya kuwa hapo alipo. Kifike kipindi awaeleze mameneja wake “HAPANA! TANZANIA NI NYUMBANI NA HAWA NI NDUGU ZANGU”
Basi kama waandaaji watashindwa kumudu gharama zake sababu Naseeb ni mfanyabiashara kama mimi, basi afanye shoo ya kujitolea (Charity show) kama tuliyofanya naye huko Tandale huko Mwanza, Kigoma, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro kwenye viwanja kwa kiingilio cha shilingi 3000 na kisha fedha hizo azipeleke kusaidia watu wanaoishi kwenye mazingira magumu na hiyo itamfanya kupendwa na mashabiki na kumfanya kwenda juu kimuziki.
TOFAUTI NA HAPA, MBELE YAKE KUNA SHIMO, UKIMYA WAKE BILA SHOO NYUMBANI UTAMZAMISHA!! MWISHO.