SAA mbili kasorobo, Mustafa baada ya kufika ofisini, kabla ya kuanza kazi haja ilimshika na kuelekea msalani.
Baada ya kumaliza kujisaidia alikwenda kwenye sinki la kusafishia mikono ili ajisafishe. Alivua pete ya ndoa na kuiweka juu ya sinki kisha alijimwagia sabuni ya maji mikononi na kuanza kunawa.
Simu iliyokuwa mfukoni ilianza kuita, kwa vile hakuweka mlio ilitetemeka kuonesha ilikuwa inaita. Hakuipokea kwa vile bado alikuwa na sabuni mikononi, hivyo alinawa haraka na kufuta mikono kwa taulo dogo ili apokee simu. Lakini kabla hajaipokea ilikuwa tayari imekatika.
Ingawa ilikuwa imekatika lakini aliitoa ili aangalie nani aliyekuwa akimpigia, kabla hajaangalia simu iliita tena, kwa vile ilikuwa mkononi aliangalia na kukuta jina la Shehna.
Japokuwa alishtuka kuona jina lile ambalo kwake lilikuwa geni. Aliamini kuzungumza na aliyepiga angemjua kwa vile jina lilikuwa kwenye simu yake.
Alibonyeza kitufe cha kupokelea na kusema:
"Haloo."
"Haloo Mustafa, asalam aleiykum," ilikuwa sauti ya lafudhi ya kimwambao.
"Waleiykum msalaam," Mustafa aliitikia huku akiifikiria sauti ile na kutaka kumjua aliyempigia ambaye jina na sauti yake vilikuwa vigeni akilini mwake.
"Upo wapi?" sauti ilimuuliza.
"Nipo ofisini."
"Nipo ofisini kwako muda tu, lakini mwenyeji wangu sikuoni."
"Nakuja basi."
"Fanya haraka kuna sehemu nawahi, nilipita ofisini kwako mara moja."
Mustafa alitoka haraka kumuwahi mgeni huyo, alimpita sekretari wake bila kumuuliza kitu japokuwa haikuwa utaratibu mzuri kumruhusu mgeni aingie ofisini bila mwenyewe kuwepo. Mara zote sekretari wake alikuwa akimruhusu mtu kuingia pale aliporuhusiwa kufanya hivyo.
Lakini kwa kauli ya mgeni kuingia ofisini ilionesha ameruhusiwa bila ridhaa yake.
Alipoingia ndani alishtuka alipokuta hakuna mtu ofisini, lakini harufu ya manukato mazuri ilisambaa kila kona.
Alitoka haraka ili amuwahi kwa kuamini huenda aliamua kutoka baada ya kuchoka kumsubiri. Lakini aliamini hakutumia muda mrefu msalani.
Alikwenda hadi getini kwa mlinzi na kumuulizia.
"Eti kuna mgeni ametoka sasa hivi?"
"Mgeni! mgeni gani?" mlinzi ilionesha kushtuka.
"Mwanamke."
"Bosi, toka uingie wewe hajaingia mtu yeyote."
Itaendelea risasi Jumamosi.
"Hapana, labda ulitoka eneo la kazi, mgeni alikuwa ofisini kwangu sasa hivi."
"Bosi hakuna mgeni yeyote zaidi ya dada Sara ambaye alikutangulia kuingia kabla yako."
"Mmh! Hebu ngoja."
Mustafa alirudi hadi ofisini na kumuuliza Sara, sekretari wake akuyekuwa bize na kazi kwenye kompyuta.
"Sasa mgeni ametoka?"
"Mgeni gani?" Sara naye alionesha kushtuka.
"Aliyekuwa ofisini kwangu sasa hivi?"
"Bosi, hakuna mgeni yeyote aliyefika hapa, kwanza ilianza lini nimruhusu mgeni aingie ofisini kwako bila ruhusa yako?"
"Sasa huyu mgeni kaingiaje na kapitia wapi?"
"Bosi mgeni unayemsema umemuona wapi?"
"Hebu njoo ofisini."
Sara na Mustafa waliongozana hadi ofisini ambako harufu ya manukato makali ilikuwa bado ikinukia.
"Bosi pafyumu nzuri kama hii umeitoa wapi?" Sara alisema huku akinyanyua pua zake kuivuta.
"Sara, haya manukato nimeyakuta baada ya kurudi kutoka msalani."
"Muongo!" Sara alishangaa.
"Kweli kabisa, yanaonekana ni ya huyo mgeni aliyeingia ofisini kwangu."
"Sasa kapitia wapi?"
"Hebu subiri."
Mustafa alisema huku akichukua simu yake juu ya meza, aliangalia namba iliyoingia yenye jina la Shehna na kuipiga. Simu ilionekana kuwa bize inazungumza.
"Simu yake inaongea."
"Mmh! Si ulitoka nje, mlinzi anasema kuna mgeni aliingia?"
"Hata yeye anasema hajamuona."
"Mmh! Mtu gani tusimuone wote basi atakuwa jini."
"Hapana si jini, nitampigia tena."
Mustafa aliachana na mambo ya mgeni asiyeonekana, alikumbuka amesahau pete yake msalani wakati akimuwahi mgeni. Alikwenda hadi sehemu ya kunawia mkono, alishtuka kukutana tena na harufu ya manukato aliyokutana nayo ofisini kwake.
Alipoangalia juu sinki hakuiona pete yake.
Alishtuka na kuangalia chini labda imeanguka vilevile hakuiona, aliingia msalani kuitafuta pia huko hakuiona.
Akili yake ilimweleza kuwa pete ile aliivua wakati akitaka kunawa mikono. Alitoka hadi kwa Sara kumuulizia.
"Sara kuna mtu ameingia msalani wakati nlipoingia ofisini?"
"Hakuna."
"Unajua wakati nanawa niliweka pete yangu ya ndoa juu ya sinki, baada ya kuzungumza na simu niliwahi ofisini lakini ajabu nimerudi sijaikuta."
"Mmh! Umeangalia vizuri?"
"Nimeangalia, Sara au leo sikuja na pete?"
"Umekuja nayo, si unakumbuka nilikutania siku ukiipoteza utamwambia nini mkeo."
"Nakumbuka, sasa imekwenda wapi?"
"Mmh! Mbona mauzauza leo."
"Huwezi kuamini ile harufu ya manukato nimekutana nayo tena msalani."
"Wewe!" Sara alishangaa.
"Kweli Sara."
"Bosi, hebu tulia kwanza inawezekana leo umeamka na mawazo mengi kutokana na ishu ya wifi. Nilikueleza mkienda Mbagala kila kitu kitakuwa sawa, yule mama kawasaidia wengi. Sema bosi tatizo ulilificha sasa hivi ungekuwa na mtoto."
"Ni kweli, jana niliporudi nimemkuta wifi yako analia."
"Tatizo?"
"Lilelile la mtoto, anasema sijui kawasikia watu wakimsema kwa mafumbo kwamba yeye ni tasa."
"Hukumweleza tuliyozungumza jana?"
"Nimemweleza lakini anasema amechoka na uongo wa waganga, tangu tuanze kuhangaikia mtoto huu mwaka wa tano sasa."
"Mwaka wa tano?" Sara alishtuka.
"Ndiyo, na fedha tulizopoteza tungeweza kujenga nyumba kubwa na gari mbili."
"Bosi yule mama kiboko wapo waliokata tamaa kama yeye lakini walipotumia dawa zake walipata watoto."
"Mbona kuna sehemu tulikwenda na kuelezwa hivyohivyo mpaka waliopata watoto tuliwaona, lakini alipotumia hakupata kitu."
"Hebu nendeni Mbagala tuone."
"Alikubali kwa shingo upande, hivi namsubiri amesema atanipitia saa tano tuelekee huko Mbagala."
"Basi bosi kapumzishe akili labda baadaye utakumbuka ulipoiweka pete."
Mustafa alirudi ofisini kwake na kukaa kitini, alijitazama vidole vyake asiamini kama kweli hakuja na pete.
Akiwa bado anavishangaa vidole vyake simu yake iliita, alipoangalia alikutana na jina la Shehna. Aliipokea:
Itaendelea tu Mkuinipatia (Like) Zenu ninawangojea ...........................